Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu , ICC, imemuhukumu kiongozi wa zamani wa kivita , pia kiongozi wa chama cha MLC Jean-Pierre Bemba kifungo cha miezi 12 kwa kosa la kuhonga mashahidi katika kesi iliyokua ikimkabili ICC.
Awali serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilitishia kuitoa nchi hiyo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC kutokana na kesi hiyo, ikishtumu utendaji kazi wa ICC, huku ikilaumu kwamba mahakama hiyo imekua ikipata shinikizo kutoka kwa baadhi ya nchi 
Wizara ya mambo ya nje ya DRC ilishtumu kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC imekua sasa ni chombo kinachonufaisha baadhi ya mataifa na kuyakandamiza mataifa mengine.
Mahakama ya Katiba ilithibitisha uamuzi wa CENI wa kumzuia Jean- Pierre Bemba kuwania katika uchaguzi wa urais wa Desemba 23 na kusema kuwa hana sifa ya kuwania katika uchaguzi huo kufuatia hukumu aliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa kosa la kuhonga mashahidi.
Jean-Pierre Bemba anatajwa kama mpinzani mkuu anayesumbua utawala wa Joseph Kabila na chama chake cha PPRD katika uchaguzi ujao.
Hivi karibuni Bemba aliachiliwa katika kesi yake dhidi ya uhalifu wa kivita na mahakama baada ya kutumikia kifungo cha miaka kumi jela.
Mwezi uliopita alirejea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kupokelewa kwa mapokezi makubwa kutoka kwa wafuasi wake.

Share with Others