Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Kikao Maalum cha Kamati Kuu iliyoketi Jumatatu, Septemba 10, 2018, jijini Dar es Salaam, kimemteua Ndugu Juma Rashid Upinde kuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Liwale, katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 13, mwaka huu.

Kamati Kuu ya CHADEMA imefanya uteuzi huo kutokana na mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya mwaka 2006, toleo la mwaka 2016, ibara ya 7.7.16(q).

Ndugu Upinde ni mmoja wa wanachama waandamizi wa CHADEMA Kanda ya Kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma) akiwa ameshiriki kukijenga na kukiimarisha chama katika maeneo hayo kupitia shughuli na harakati mbalimbali kwa muda mrefu.

Mgombea huyo wa CHADEMA Ndugu Upinde tayari ameshachukua fomu ya kugombea ubunge na kukamilisha kuijaza ambapo asubuhi hii anairejesha kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Liwale kwa ajili ya uteuzi utakaofanyika leo Alhamis, Septemba 13, ifikapo saa 10.00 jioni. Kampeni za uchaguzi huo zitaanza Septemba 14 hadi Oktoba 12, mwaka huu.

Ili kujihakikishia ushindi katika uchaguzi huo, kupitia kikao hicho pia imeazimiwa kuwa Chama na mgombea huyo watazingatia maslahi na matakwa ya wananchi hasa kupitia ushirikiano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Imetolewa leo Alhamis, Septemba 13, 2018 na;

Share with Others