Dar es Salaam ni mji wa pili Afrika mashariki kwa utajiri baada ya Nairobi, ambapo kwa jumla Afrika ni mji wa 12 na Nairobi mji wa sita huku Mombasa ukiwa ni mji wa 23 kwa utajiri Afrika.
Tanzania ni Taifa la nane kwa utajiri wa raia wake barani Afrika, ambapo Kenya inashikilia nafasi ya tano.
Kwa mujibu wa ripoti ya New World Wealth pamoja na benki ya AfrAsia nchini Mauritius, utajiri wa Dar es Salaam wenye thamani ya $25 bn mwaka 2017 umetokana na viwango vya utajiri wa watu binafsi (HNWIs) na pia mapato yanayoingia katika sekta ya starehe barani Afrika kama hoteli na vivutio vingine.
Hii ni hatua iliyopigwa ikilinganishwa na utajiri wa thamani ya $23bn kwa nchi nzima ya Tanzania mnamo mwaka 2011.
Kwa jumla ripoti hiyo inakadiria kuwa sekta hiyo ya starehe barani Afrika imechangia takriban $ bilioni 6.0 za mapato mnamo 2017.
Katika ongezeko la utajiri, mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, isipokuwa Burundi, ni miongoni mwa nchi ambazo zimeimarika pakubwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita huku Mauritius ikiongoza kwa ukuaji wa asilimia 192 ikifuatwa na Ethiopia iliyokuwa kwa asilimia 190.
Mataifa ya Afrika Mashariki  yanaongozwa na Rwanda (74%), Kenya (73%), Tanzania (66%), na Uganda (53%), takwimu hii inajumuisha vitu kama  Magari, nguo za kifahari, ndege za kibinafsi, maboti , na hoteli zinazomilikiwa.
Afrika kusini ni kivutio kikuu cha utalii Afrika, lakini Tanzania inasifika pakubwa kwa vivutio vikiwemo  Ngorongoro na mbuga ya Serengeti.
 

Share with Others