Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini.
Kwa mujibu wa EWURA, mwezi huu bei hizo zimeongezeka, ikilinganishwa na mwezi uliopita.

 

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Godfrey Chibulunje imebainisha kuwa bei hizo mpya, zitaanza kutumika kuanzia leo.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa Septemba bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa, zimeongezeka kwa Sh 20 kwa lita (sawa na asilimia 1.11), Sh nane kwa lita (sawa na asilimia 0.46) na Sh 124 kwa lita (sawa na asilimia 7.93).

 

Taarifa imeeleza kuwa, mwezi huu bei za rejareja na jumla kwa bidhaa za mafuta ya Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kusini (Lindi, Mtwara and Ruvuma) zimeongezeka ikilinganisha na bei zilizotolewa mwezi uliopita.

 

Ilibainisha kuwa mwezi huu, bei hizo za rejareja za Petroli na Dizeli zimeongezeka kwa Sh 11 kwa lita (sawa na asilimia 0.60) na Sh 16 kwa lita (sawa na asilimia 0.91), mtawalia.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo vilevile, ukilinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za Petroli na Dizeli zimeongezeka kwa Sh 11.19 kwa lita (sawa na asilimia 0.64) na Sh 16.36/lita (sawa na asilimia 0.98).

 

Alisema mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani, yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji na gharama za ucheleweshaji wa ushushaji wa mafuta.

 

Taarifa ya Chibulunje imesisitiza kuwa kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani, ilimradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (kama ilivyokokotolewa na kanuni iliyopitishwa na Ewura na ambayo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali Namba 74 la Februari mwaka huu).

Share with Others