Watoto wawili wa familia moja wameuawa kikatili katika Kitongoji cha Kwazoka wilayani Kibaha mkoani Pwani, baada ya kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Yasin Abdala kuvamia nyumbani kwao na kisha kuwakata kwa panga.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amesema kuwa tukio hilo limetokea baada ya kijana huyo anayefanya kazi za ndani jirani na eneo hilo kuvamia nyumbani kwa mama mzazi wa watoto hao, Saada Maulidi ambaye pia amejeruhiwa.

Amewataja watoto hao kuwa ni Rehema Makolo mwenye umri wa miaka mitano na mwanafunzi wa darasa la awali katika shule ya Kwazoka na Abubakari Makolo mwenye umri wa miaka sita ambae ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi kwazoka.

Kamanda Wankyo amesema kuwa baada ya mauaji hayo baadhi ya majirani walifika nyumbani kwa mwanamke huyo na kumkamata kijana huyo na kwenda kumfungia katika ofisi ya Kijiji cha Kwazoka.

Amesema akiwa ndani ya ofisi hiyo, kijana huyo alivunja mlango na kukimbia na ndipo wakafanikiwa kumkamata tena na kumshambuliwa kwa kutumia za zana za jadi ambapo baadae alifariki dunia.

Mama mzazi wa watoto hao amelazwa katika Kituo cha Afya cha Mlandizi huku hali yake ikielezwa kuwa ni mbaya na miili ya watoto hao ikiwa imehifadhiwa katika kituo hicho afya.

Share with Others