Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imewafikisha mahakamani watu watano wakituhumiwa kujipatia fedha Sh 58,335,260 Milioni za wakulima wa Korosho katika Chama cha Ushirika cha Msingi cha Umoja kilichopo Wilayani Liwale Mkoani humo.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Lindi Abenery Mganga leo Machi 16,2021 amesema,hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanya uchunguzi kufuatia kupata taarifa za siri mnamo Agosti 24 mwaka 2020 zilizolalamikia upotevu wa tani 200 za korosho kwenye ghala la chama hicho na kusababisha chama kushindwa kuwalipa wakulima fedha zao katika msimu wa korosho wa mwaka 2019/2020.

Miongoni mwa watuhumiwa hao waliotajwa na Mkuu wa Takukuru ni pamoja na Rahim Hamis Tewele (Katibu Mkuu) mwenye jukumu la kuandaa na kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakulima ambapo imetajwa kuwa alitumia mwanya huo vibaya kinyume na sheria kwa kughushi nyaraka na kuingiza majina ya ndugu zake akijua watu hao hawakuwahi kuuza korosho zao kwenye msimu wa 2019/2020.

Mganga ameweka wazi kuwa mtuhumiwa Tewele aliingiza jina la mdogo wake Abdulatif Hamis Tewele,rafiki yake Said Ally mkazi wa Kijiji cha Mbonde,Hawa Salum(mama yake)na mfanyakazi mwenzake Kuruthum Hassan Mfaume na kwamba majina hayo yote yaliingizwa kwenye orodha ya wanaostahili kulipwa mnada wa 7 na 8,kitendo kilichosababisha watuhumiwa hao kupokea malipo haramu ya Sh Mil 58,335,260,kulingana na stahiki zao zilizoandikwa.

Aidha,Mganga ametoa rai kwa watumishi wote wa Serikali na Sekta binafsi katika Mkoa wa Lindi kuwa kila mmoja anatakiwa kuendelea kuzingatia viapo vya utumishi na maadili ya kazi na Takukuru itaendelea kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafikisha mahakamani watakaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Share with Others