Mwili wa aliyekuwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan unatarajiwa kuzikwa hii leo katika mji mkuu wa Ghana, Accra.
Kwa muda wa siku mbili zilizopita mwili wake ulikuwa ukiagwa mjini humo na watu mbalimbali, wakiwemo watu maarufu.
Viongozi kadhaa wa nchi wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo katika makaburi ya jeshi ya Kambi ya Burma mjini Accra.
Kofi Annan alihudumu kama Katibu Mkuu wa saba wa Umoja wa Mataifa kati ya 1997 na 2006.
Leo inahitimisha kilele cha wiki kadhaa ya maandalizi ya mazishi yake, ambaye ni mmoja kati ya wana diplomasia wanaoheshimika duniani.
Miongoni mwa waombolezaji hao ambaye tayari amewasili mjini humo ni aliyewahi kuwa mke wa Rais wa kwanza wa Afrika kusini Nelson Mandela, Bi. Graca Machel.
 

Share with Others