Chama kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao, kimefanya uchaguzi kupitia mkutano wake Mkuu na kuwachagua viongozi wapya 7 wa bodi wa chama hicho kutoka Kilwa,Lindi Manispaa na Mtama watakaoongoza katika kipindi cha miaka 3 baada ya waliokuwepo kumaliza muda wao.

Uchaguzi huo ulioshuhudiwa na viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Lindi GODFREY ZAMBI, Mrajisi msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Lindi EDMUND MASAWE na mwakilishi kutoka tume ya maendeleo ya ushirika TCDC, BARAKA LUKIO  umefanyika Mjini Lindi, ambapo jumla ya wajumbe 101 kati ya 102 wa mkutano mkuu wa Lindi Mwambao wamepiga kura.

Katika uchaguzi huo,wajumbe watatu wapya wa bodi , ISMAIL NALINGA kutoka Kingoli Amcos Kilwa, MBELA HASSAN (Mtua) na   CHARLES MKOPOLA (Nyengedi) walijitokeza kuwania nafasi ya Uwenyekiti huku mjumbe mmoja YASIN HASHIMU nae kutoka Kilwa akijitokeza kuwania umakamu mwenyekiti.

Aidha,kati ya kura halali 99 zilizopigwa kura 45 zilimpa ushindi ISMAIL NALINGA kuwa mwenyekiti mpya wa bodi ya Lindi Mwambao akiwashinda wapinzani wake Mbela Hassan na Charles Mkopola waliofungana kwa kura 27.

Wakizungumza baada ya uchaguzi kumalizika wajumbe wa Mkutano mkuu huo wamewakumbusha viongozi hao kusimama kidete kutetea masahi ya wakulima wakati mwenyekiti mpya wa Bodi ISMAIL NALINGA akiahidi kushirikiana na wadau wote wa ushirika ili kuleta tija.

Share with Others