Maandamano yaliyosababishwa na kifo cha Mmarekani mweusi, George Floyd yamepelekea Jimbo la Washington kutangaza muda wa wananchi kubaki ndani baada ya maandamano kufanyika karibu na Ikulu (White House)

Kutokana na vurugu zilizokuwa zikiendelea nje ya White House, imeelezwa kuwa Usalama wa Taifa walimpeleka Rais Donald Trump kwenye chumba cha chini cha ardhi ambacho kilitumika wakati wa mashambulio ya kigaidi zamani

Mabomu ya machozi yametumika kutawanya waandamanaji zaidi ya 1,000 waliokuwa nje ya Ikulu na mabango huku wakiimba na kuwasha moto. Tangu kuanza kwa maandamano, inadaiwa takriban watu 4,100 wamekamatwa kutokana na makosa ya kuvunja maduka, kufunga barabara na kutozingatia muda wa kutotoka ndani

Mamlaka zimeweka zuio la muda wa kubaki ndani Washington pamoja na miji mingine mikubwa ikiwemo Atlanta, Chicago, Denver, Los Angeles, San Francisco na Seattle ili kudhibiti waandamanaji wanaopinga ukatili unaofanywa na Polisi kwa watu weusi 

George Floyd alifariki dunia Jumatatu iliyopita Mei 25, 2020 huko Minneapolis baada ya Polisi mzungu, Derek Chauvin kumkandamiza shingoni kwa kutumia goti. Tangu tukio hilo, Chauvin pamoja na maafisa wengine watatu waliokuwepo wamefukuzwa kazi

Aidha Chauvin amefunguliwa mashtaka ya mauaji daraja la tatu lakini waandamanaji wameendelea kudai hiyo haitoshi huku wakitaka Polisi wengine watatu waliokuwepo kushtakiwa 

Share with Others