Serikali kupitia wizara ya kilimo imesitisha kwa muda mwongozo uliotolewa awali wa wakulima wa korosho kukatwa Sh 110 kwa kila kg 1 ya korosho kwaajili ya pembejeo mpaka kitakapofanyika kikao cha wadau wa korosho juni 6,2021 Mkoani Lindi.


Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu KASSIM MAJALIWA leo Juni 3,2021 bungeni Jijini Dodoma wakati wa  kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa waziri Mkuu.


Kauli hiyo ya Waziri Mkuu MAJALIWA imekuja kufuatia Mbunge wa jimbo la Liwale ZUBERI KUCHAUKA kuuliza swali kuhusu zao la korosho akilenga taharuki iliyowakuta wakulima baada ya bodi ya korosho kutoa waraka unaoeleza mkulima wa korosho atakayepeleka korosho kwenye mnada atakatwa Shilingi 110 na atalipia akishauza korosho hizo.Akieleza juu ya hilo,Waziri mkuu Majaliwa amekiri kuwepo kwa taharuki kwa wakulima wa korosho iliyotokana na vikao vya awali vya majadiliano ya namna nzuri ya kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji,vikao ambavyo amesema havijakamilika hivyo kupitia kikao kikubwa kitakachofanyika tarehe 6  kitakachowahusisha na wakulima watajadili kiundani.


Aidha,amesema kwakua tayari pembejeo zimeshapelekwa kwenye Amcos wakulima wasisite kuzipokea kwani kikao hicho kitatoa mwelekeo mzuri juu ya nini kitafanyika kwa pembejeo ambazo zimetolewa.

 

Share with Others