Wakulima wa Korosho wilaya ya Tandahimba na Newala leo wameuza Korosho zao tani 13,181kwa bei ya juu ya shilingi 2526 kwa kilo moja huku bei ya chini ikiwa shilingi 2468 kwenye mnada wa kwanza wa chama Kikuu cha Ushirika TANECU ,uliofanyika Mjini Newala.


Taarifa ya makusanyo ya Korosho na kiasi kilichoingizwa katika mnada iliyosomwa na meneja mkuu wa TANECU Bw.Mohammed Nassoro  imebainisha kuwa Korosho zilizouzwa zilikuwa kwenye maghala makuu ya TANECU yaliyopo Newala na Tandahimba na Agrofocus Newala. Aidha la Agrofocus zimeuzwa tani 194, ghala la Tanecu Newala zimeuzwa tani 6,303 na ghala la Tanecu Tandahimba zimeuzwa tani 6,682.


Wakulima walifikia maamuzi ya kuuza Korosho zao baada ya kaimu mkurugenzi Bodi ya Korosho Tanzania, Frances Alfred  kutoa taarifa ya bei ya korosho soko la Duniani hadi kufikia leo kuwa Korosho inauzwa kati ya shilingi 2440 hadi shilingi 2740.


Mnada wa leo ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali akiwemo Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe.Gelasius Byakanwa ambaye amewasisitiza viongozi wa chama Kikuu cha Tanecu ltd na Bodi ya Korosho Tanzania kuharakisha mchakato wa malipo ili wakulima walipwe fedha zao kwa muda muafaka.


Aidha kampuni 28 zilijitokeza kuomba kununua Korosho ambapo hitaji ilikuwa kununua Korosho tani 40,000 lakini makusanyo ya Korosho na kiasi kilichoingizwa katika mnada hadi kufikia oktoba 29,mwaka huu kilikuwa tani 13,181.

Share with Others