Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema kuwa amefanya uchunguzi na kubaini mchezo mchafu katika vipimo vya virusi vya corona, vilivyofanywa na Maabara Kuu ya Taifa (National Referral Laboratory).

Akizungumza leo, Mei 3, 2020 katika hafla ya kumuapisha Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Rais Magufuli amesema kuwa baada ya kuona majibu mengi ya vipimo vya sampuli za watu yanaonesha wameathirika, aliamua kufanya uchunguzi wa siri kwa kutumia vyombo vya usalama na timu maalum ya wataalam aliowateua.

Rais amesema kwamba timu hiyo iliwasilisha sampuli za vitu mbalimbali ambavyo sio binadamu na kuvipa majina ya binadamu ili kubaini kinachoendelea. Baadhi ya vitu hivyo ni pamoja na papai, fenesi, kware, mbuzi vilikutwa na virusi vya corona.

“Sample ya oili ya gari kwa mfano tuliipa jina la Jabir Hamza mwenye miaka 30 (mwanaume), ile ilileta negative (haikuwa na maambukizi), tulipopeleka sample ya fenesi ambayo tuliipa jina la Sara Samweli mwenye miaka 45 (mwanamke), matokeo yake yalikuwa ‘inconclusive’. Tulipopeleka sample ya papai, tukaipa jina la Elizabeth Anne miaka 26 (mwanamke), papai lile lilikuwa positive… kwamba lina corona. Maana yake maji yaliyotolewa mle kwenye papai ni positive (yameathirika),” amesema Rais Magufuli.

“Tulipeleka sample ya ndege kware imekuwa positive, tumechukua mbuzi akawa positive, tukachukua kondoo akawa negative, n.k,” aliongeza.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli amesema kuna tatizo katika masuala ya vipimo vya corona huku akitilia shaka vifaa vinavyotumika.

“Huenda hizi mashine za vipimo, zimeweka zikipima vipimo kadhaa inayofuata lazima iwe positive. Hili nalo lazima liangaliwe. Nilishasema tusikubali kila msaada tukafikiri ni kwa faida ya nchi. Na ndio maana wengi wanaoambiwa wana corona ni wazima tu wala hawasikii kitu kingine. Of course mnaweza kusema labda kinga zao za mwili ziko juu, ni sawa… lakini haya yote tuyaangalie,” ameongeza.

Aidha Magufuli ametoa wito kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) na nchi za Afrika kuchukua hatua na kuliangalia suala hili kwa undani huku akiwataka kufanya majaribio kwa vitu vingine ili wabaini kile alichokibaini.

Pamoja na hayo Rais Magufu amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi na kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona mbapo maesema kuwa ugonjwa huu utapita kama magonjwa mengine huku akisema anafikiria kutoa ruhusa ya kufunguliwa kwa Ligi za michezo mbalimbali kwani inaonekana watu wanaoshiriki michezo na kufanya mazoezi hawaathiriki zaidi na ugonjwa huu.

Aidha amewataka wanasiasa kutotumia ugonjwa huu kama mtaji wa kisiasa kwani hautawasaidia.

Share with Others