Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi katika kuhakikisha Mkoa huo unaongeza uzalishaji wa Korosho amemuagiza katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Rehema Madenge kuzipa viwango vya uzalishaji wa miche ya mikorosho  halmashauri Mkoani humo ikienda sambamba na uanzishaji wa mashamba ya mikorosho ili kufikia lengo la Mkoa kuzalisha miche Milioni 1 kwa mwaka.

 

Zambi ametoa kauli hiyo katika kikao cha tathimini ya msimu wa korosho kwa mwaka 2020/21 ambapo zimebainika baadhi ya halmashauri kuzalisha miche ya mikorosho kwa kiwango cha chini na kusababisha lengo la Mkoa  kutofikiwa.

 


Awali wakitoa tathimini ya uzalishaji wa miche ya korosho katika halmashauri zao, Wakurugenzi katika halmashauri zilizopo mkoani humo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea Hassan Rugwa amesema katika kipindi cha miaka mitano halmashauri hiyo imezalisha miche ya Mikorosho zaidi ya 150,000 sawa na wastani wa hekari 6,000 huku kwa mwaka 2021 pekee wakizalisha miche  37,000.


Amesema kati ya miche hiyo 37,000, Miche  17,000 ilikuwa ni kutoka kwa wadau binafsi, 20,000  imezalishwa na halmashauri na kuwapa wakulima ambapo kiasi cha Sh Mil 10 kilitengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

 

Nae, Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Renatus Mchau licha ya kuweka wazi  Mbele ya wajumbe  katika kikao hicho idadi ya miche waliyozalisha ameeleza pia kuwa wapo kwenye mchakato wa kuanzisha mradi wa shamba la mikorosho la halmashauri eneo la Kikole lenye ukubwa wa hekari 1,000.

 

 

Kwa upande wa Manispaa ya Lindi, Mkurugenzi wa manispaa hiyo Jomari Satura katika msimu uliopita wa korosho amesema wamezalisha miche  120,000 na kutumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji ambao wangependa kuwekeza katika kilimo kwani wanayo maeneo ya kutosha yanayofaa kwa shuguli za kilimo ikiwemo kilimo cha korosho.

Share with Others