Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limekanusha taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Katibu wa CHADEMA wa wilaya ya Ruangwa, CLAUDIO TEODORI CHILEMBA ametekwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Ruangwa leo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, STANLEY KULYAMO amesema hakuna taarifa zozote za utekaji nyara kwa mtu huyo.

Amesema kuwa Jeshi la Polisi liliwasiliana na Msimamizi wa CHADEMA wa Kanda ya Kusini, STEWARD ERNEST KAKINGI ambaye alithibitisha kuwepo kwa katibu huyo wilayani Masasi na aliahidi kumpeleka Kituo cha Polisi kwa mahojiano akiwa na Mwanasheria wa Chama hicho ingawa hadi sasa hajafanya hivyo.

Kamanda KULYAMO amesema kupitia kwa wasiri wake, jana Jeshi la Polisi lilipata taarifa kwamba CHILEMBA amekwishachukua fomu za kuwania kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea udiwani kata ya Chienjele wilayani Ruangwa kwa tiketi ya CHADEMA.

Wakati huo huo, Kamanda Kulyamo amesema vijana watatu wamekatwa eneo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ruangwa wakiwa na nondo mbili zilizoviringishwa bendera mbili za Chama cha ACT WAZALENDO pamoja na kisu kimoja na majina yao yamehifadhiwa.

Kamanda KULYAMO amesema kati ya vijana hao, wawili wametoka Manispaa ya Lindi na mmoja ametoka Kata ya Mbekenyera ambapo kwa sasa wote watatu wako chini ya ulinzi wa jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.

Share with Others