SERIKALI imetoa waraka wa mwongozo mpya kuhusu uendeshaji wa taasisi za kidini nchini wenye mambo tisa ya kuzingatia. Pia, imeonya na kuyabana zaidi madhehebu yanaoibuka bila kuwa na mifumo mizuri ya kitaasisi, yanayotumia usajili wa wengine na wanaoruhusu usajili wao kutumiwa bila kufuata sheria.

Waraka huo pia umegusa eneo la ruhusa ya mikutano ya hadhara, ambayo sasa itatolewa kwa taasisi au jumuiya ya dini, iliyosajiliwa tu au kwa kibali maalum cha Msajili wa Jumuiya za Kijamii.

Baada ya serikali kutoa waraka huo kwa umma, uliosainiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene,  viongozi wa dini wamesema hatua hiyo ya serikali ni sahihi, kwa kuwa kila uhuru popote duniani, una utaratibu wake unaozingatia sheria za nchi husika.

Katika mwongozo huo, maelekezo ya serikali yamezingatia uwepo wa tabia ya watu kuanzisha na kuendesha taasisi au jumuiya za kidini, bila kuzingatia sheria za nchi na vibali vyao na bila kuwa na usajili au kibali cha kuendesha shughuli zake.

Mambo ya kuzingatia yaliyoainishwa katika mwongozo huo ni kuhakikisha taasisi au jumuiya, zimesajiliwa au zina ruhusa ya kufanya shughuli zake kutoka kwa Msajili wa Jumuiya za Kijamii Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

“Kila taasisi au jumuiya ya kidini ihakikishe kuwa ina orodha ya matawi yake yote nchini na viongozi wa matawi hayo. Hii ni pamoja na kuwa na utaratibu wa kitaasisi unaotumika katika kusimamia matawi hayo na kuwadhibiti viongozi na waumini wao katika matawi hayo,” ilieleza sehemu ya maelekezo hayo.

Aidha, maelekezo hayo yametaka kila taasisi au jumuiya kuwa na mpango wa mafunzo kwa watumishi wake ili kuwajengea uwezo na weledi, utakaowasaidia katika shughuli zao za kila siku. Eneo jingine ni kila taasisi au jumuiya, inapofanya mikutano yenye watu wengi, izingatie usalama wa watu hao na kuweka tahadhari za kujikinga na hatari yoyote, inayoweza kutokea kwenye mikutano hiyo.

“Kila nyumba ya ibada inapaswa kuwa na vifaa vya kujikinga na majanga yanayoweza kuhatarisha maisha ya watu mfano vifaa vya kuzima moto na milango ya dharura itakayowezesha watu kutoka kwa haraka ndani ya jengo endapo kutakuwa na hatari yoyote,” ilielekeza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa maelekezo hayo ya serikali, kwenye mikutano ya hadhara viongozi wanapaswa kuzingatia muda wa kuanza na kumaliza mikutano hiyo, kama ilivyoainishwa kwenye kibali cha kuifanya, huku ruhusa ya kuendesha mikutano ya hadhara, ikitolewa kwa taasisi zilizosajiliwa tu au kwa kibali cha Msajili wa Jumuiya za Kijamii.

Serikali imeagiza kupitia maelekezo yake kuwa taasisi zote za kidini, zinazotumia usajili wa taasisi zingine ziripoti mara moja kwa Msajili wa Jumuiya za Kijamii Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa maelekezo na taasisi au jumuiya kuacha mara moja tabia ya kuruhusu usajili wake kutumiwa na taasisi nyingine kwa makubaliano yasioridhiwa na serikali.

Serikali pia katika waraka huo imeeleza kuwa hatua hiyo inatokana na uwepo wa changamoto mbalimbali, ikiwamo baadhi ya taasisi hizo kutozingatia masharti ya vibali vya serikali, kuendesha shughuli bila kusajiliwa na zilizosajiliwa kutokuwa na utaratibu mzuri wa kitaasisi wa kuendesha shughuli zao.

Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima amesema kuwa hatua hiyo ya serikali ni sahihi, kwa kuwa inaweka misingi ya kuheshimu sheria za nchi, hivyo kila dhehebu kwa misingi ya kuanzishwa kwake, linapaswa kujiangalia upya, ikiwa linazingatia sheria za Mungu na za nchi.

“Nimepokea barua hii na ninaisambaza kwa maaskofu wa majimbo yote ya Katoliki. Ni kweli Ibara ya 19 ya Katiba ya nchi inatoa uhuru wa kuamini unachokitaka ila kwa kuzingatia sheria za nchi, hivyo waraka huu unatuhitaji kila dhehebu lijiangalie na kujipima ni taasisi au ni mtu.

Haiwezekani mtu akawa yeye mchungaji, yeye mhasibu, yeye mtawala, lazima kuwepo na mgawanyo wa kazi unaoliweka dhehebu katika mfumo wa kitaasisi na si wa mtu mmoja. Si sahihi kujisajili kwa mgongo wa dhehebu jingine, kama kweli unajitosheleza, kwanini uegemee kwa mtu?,” alihoji Padri Kitima.

Share with Others