Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limewafutia matokeo watahiniwa 1,059 kutoka shule 38 zilizofanya udanganyifu katika mitihani ya kuhitimu darasa la saba mwaka huu.


Akitangaza matokeo hayo leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde amesema watahiniwa hao hawatapata nafasi nyingine ya kurudia mitihani hiyo.


Msonde amesema pamoja na kamati ya mitihani kutimiza wajibu wao vizuri, kumejitokeza matukio machache ya udanganyifu wa mitihani katika baadhi ya shule nchini ambapo jumla ya shule 38 sawa na asilimia 0.22 ya shule zote za msingi 17,329 zilizofanya mitihani,zimebainika kufanya udanganyifu huo.


Amesema shule hizo zilifanya makosa mbalimbali ikiwamo kuiba mitihani, kugawa majibu kwa wanafunzi na kubadilisha watahiniwa kwa kuwaweka wasio halisi kuwafanyia mitihani wanafunzi watoto.


Shule zilizobainika kufanya udanganyifu huo ni pamoja na Matogoro ya Tandahimba Mkoani Mtwara,Ngiloli, Nguyami, Ibuti, Ihenje,Bwawani,Mogohigwa, Chakwale, Msingisi zilizopo Halmashauri ya Gairo.


Zingine ni Mafiri, Kibogoji, Ng’wambe, Digalama, Dihinda kutoka Halmashauri ya Mvomero na shule za msingi za Nyawa A iliyopo Halmashauri ya Bariadi vijijini (Simiyu).


Shule zingine ni za Halmashauri ya Chabutwa, Sikonge Tabora ikiwemo shule ya msingi Chabutwa, Usagari, Uyui Tabora Siashimbwe iliyopo Moshi Kilimanjaro, Dominion Arusha, Ng’arita Bariadi vijijini mkoani Simiyu, Olkitikiti Kiteto iliyopo Manyara na Nyamimina Buchosa Mwanza.

Share with Others