Maafisa wa Masoko kutoka shirika la umeme Tanzania (TANESCO) makao makuu Bi. Jenifer Mgendi, Adeline Lyakulwa na Mhandisi Baraka Kanyika wakishirikiana na Afisa Uhusiano mkoa wa Lindi Francis Mbelwa wametembelea na kutoa elimu ya matumizi bora ya umeme kwenye migodi ya kuchimba dhahabu iliyopo Namungo wilayani Ruangwa katika mkoa wa Lindi.

 

Akiongea kwa niaba ya timu hiyo Bi. Jenifer Mgendi ambaye ndiyo kiongozi wa msafara huo amesema kuwa elimu ya matumizi bora ya umeme waliyoipata wachimbaji itawasaidia wateja katika kufahamu namna nzuri ya kutumia vifaa vya kisasa vinavyotumia umeme mchache na kuokoa fedha za mtumiaji ambazo anaweza kuzitumia kwa ajali ya matumizi mengine.

 

Sambamba na hiyo mhandisi Baraka Kanyika amesisitiza juu ya umuhimu wa kufunga miundombinu (wiring) ya kisasa ili kuweka usalama kwa watumiaji wa umeme kwenye viwanda vidogo vidogo mkoani humo.

 

Aidha Afisa Uhusiano wa TANESCO mkoa wa Lindi Francis Mbelwa amewashauri wateja wa shirika hilo hasa wa viwandani kuzingatia umuhimu wa kuwaita wakandarasi wanaotambulika na Tanesco ili wakague miundombinu yao kila baada ya miaka mitano au mitatu na hata chini ya muda huo kadili ya wanavyoona inafaa ili kuhakikisha mali zao zinakuwa salama 

 

Ziara hiyo ya viongozi kutoka makao makuu kwa mkoa wa Lindi ilianza Agosti 17 wilaya ya Lindi na inatarajia kumalizika wilayani Kilwa mkoani humo 

Share with Others