Ili kuhakikisha mkulima wa zao la korosho anapata pembejeo kwa wakati na kuongeza uzalishaji wa zao la Korosho, vyama vikuu vya ushirika vimepewa jukumu la kuagiza pembejeo kwa pamoja na kugawa kwa mkulima, ambapo atalipia kupitia makato yake baada ya kuuza korosho zake.


Kauli hiyo imetolewa Mkoani Lindi Mei 11,2021 na Kaimu mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis  Alfred wakati akizungumza na wanahabari kuhusu sababu zilizochangia kushuka kwa uzalishaji wa korosho kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita kutoka 2017/2018 ambako zilizalishwa Tani laki 319,600 , hadi Tani laki 210,000 kwa msimu uliopita 2020/2021.

Alfred amesema kupitia utafiti walioufanya kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa kilimo Tari Naliendele Mtwara kwenda kwa wakulima juu ya kushuka kwa uzalishaji huo,wamebaini kuwepo kwa sababu nyingi ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa yaliyochangia kuibuka kwa magonjwa na wadudu wasumbufu kwenye zao la korosho.

Sababu nyingine iliyobainika ni wakulima wengi kutumia kiasi kidogo cha pembejeo ambacho hakilingani na mahitaji yao huku wengine wakinunua viwatilifu kiholela visivyokuwa na ubora kwaajili ya kufuata unafuu wa bei.

Amesema baada ya kubainika hayo,Serikali kupitia bodi ya korosho imemua kujadiliana na wadau mbalimbali wakiwemo vyama vyama vikuu vya ushirika ili kumnusuru mkulima azalishe kwa wingi na kupata tija,ambapo wamekuja na mpango wa kuagiza pembejeo kwa pamoja na kulipia baada ya mkulima kuuza mazao yake ambapo pia wamependekeza mkulima akatwe Sh 110 kwa kila kg1 ya  korosho.

Aidha ameongeza kuwa mpango huo utampunguzia mkulima gharama kwa ununuzi wa pembejeo na kupata viwatilifu vyenye ubora kwani watahakikisha wanahakiki viwatilifu hivyo kabla ya kwenda kwa wakulima.

Share with Others