Jumla ya wazazi 35 kutoka kata ya Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wamekatwa baada ya kukutwa wakiwafundisha watoto wa kike walio chini ya umri wa miaka 8 mbinu za kuishi na wanaume na kufanya tendo la ngono maarufu kama msondo.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo alisema, wazazi hao wamekamatwa nyakati za usiku wakiwa wamejifungia kwenye nyumba ya mmoja wa waliokamatwa katika kijiji cha Nalasi wakiwa na watoto hao.

Aidha ameongeza kuwa wazazi hao wamekamatwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kwamba, kuna wazazi wamewaficha watoto wa kike wenye umri mdogo na kuwafundisha mila potofu zinazohusiana na mambo ya ngono ambayo hayapaswi kufundishwa watoto wadogo  na kusema wazazi hao walikamatwa nyakati za usiku wakiwa na watoto hao wadogo wakiwa katika moja ya nyumba iliyokuwa inatumika kwa shughuli hiyo.

Pia amesema,katika msako huo mbali na wazazi hao wamemkamata Kungwi mmoja,mtendaji wa Rajabu Lusanga na mwenyekiti wa kijiji cha Nalasi Ali Omari ambao wameshindwa kuchukua hatua dhidi ya wazazi hao licha ya kuishi jirani na eneo la tukio hilo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya  shughuli za msondo hazikatwi kufanywa, isipokuwa ni kwa wasichana wakubwa wenye umri zaidi ya miaka 18 na wale wanatarajia kuolewa, badala ya kuwafundisha watoto wadogo ambao hawana uwezo wa kuelewa jambo lolote.

“natoa wito kwa wazazi wote katika wilaya ya Tunduru tabia ya kuwafundisha watoto wadogo namna ya kuishi mama na baba jambo hilo tumelipiga marufuku kwani linachangia sana kuongezeka kwa mimba na wasichana wengi kuacha shule”alisema, Mtatiro.

Alisema, vitendo hivyo vinasababisha watoto wadogo wa kike kukosa haki yao ya kupata elimu na kusisitiza kuwa operesheni hiyo itaendelea katika vijiji mbalimbali hadi pale jamii itakapo acha kufanya vitendo hivyo.

Baadhi ya wakazi wa Tunduru wamepongeza jitihada kubwa zinazo fanywa na Serikali ikiongozwa na Mkuu wa wilaya ya kukomesha baadhi ya mira potofu ambazo zimekuwa chanzo cha kuongezeka kwa mimba kwa watoto wa kike wengine kuacha masomo.

Share with Others