Mahakama ya hakimu Mkazi Wilaya ya Lindi leo Mei 31,2021 imesogeza mbele hadi Juni 14,2021 shauri la uhujumu uchumi namba 2,2021 linalowakabili raia 7 wa Iran waliokamatwa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi April 22,2021 wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine Kg 504.36 na Methamphetamine Kg 355.

Shauri hilo limesogezwa mbele baada ya mwendesha mashtaka ambaye ni wakili msomi wa Serikali Juma Maige kuiomba mahakama kulipangia tarehe nyingine kwakuwa upelelezi bado unaendelea.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Lindi Consolatha Singano mara tu mwendesha mashtaka Juma Maige kuiomba mahakama kulitaja tena shauri hilo akaamuru washtakiwa hao 7 raia wa Iran wanaozungumza lugha ya persian kurudishwa rumande hadi juni 14,2021.

Aidha,upande wa utetezi,mawakili wake Silvanus Nyamikindo na Kheri Bahati Lowasa, licha ya maamuzi hayo ya mahakama, wakaomba ipangwe tarehe nyingine tofauti na hiyo juni 14 kwa kile walichokieleza mahakamani hapo kuwa kipindi hicho watakuwa na kesi maeneo mengine,jambo ambalo Hakimu Consolatha Singano hakubadilisha maamuzi na kueleza tarehe za mashauri zinapangwa kwa mujibu wa sheria.

Washtakiwa kwenye shauri hilo ni JAN MOHAMMAD MIRAN (42), ISSA BALUCHI AHMAD (30), AMIR HUSSEIN KASOM(35), SALIM BALUCHI FEDHMUHAMMAD (20).

Wengine ni IKBAL PAKIL MOHAMED (22),MUSTAPHAR NOWAN KADIR BAKSH(20) na JAWID NUHANNUR MOHAMED (19).

Share with Others