Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameivunja Bodi ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) iliyoteuliwa rasmi tarehe 1 Disemba 2017 ikiwa na wajumbe sita ambao ni Mhandisi Eli Pallangyo, Bw Nuru Ndile, Bi Rosemary Msabaha, Bw Peter Shao, Dkt Kadida Mashaushi na aliyekuwa Mwenyekiti Marehemu Prof Egid Mubofu.

Waziri Hasunga amefanya maamuzi hayo wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi za Kampuni hiyo ya TFC Jijini Dar es salaam.


Akizungumza katika kikao hicho Waziri Hasunga amesema kuwa ameivunja Bodi hiyo kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi hivyo kusababisha kampuni kushindwa kufanya biashara, kampuni kujiendesha kwa hasara na kushindwa kufikia matakwa ya kuanzishwa kwa kampuni hiyo ya kuwa msambazaji kiongozi na anayeaminika kwa mbolea ya pembejeo zingine nchini kwa kuzingatia mahitaji ya mazao na afya ya udongo.

Katika hatua nyingine ametengua uteuzi wa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tito Haule, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Primus Kimaryo, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Dkt Julius Ningu wote kwa pamoja ni kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Share with Others