Jumla ya vijiji 192 kati ya 524 vilivyopo Mkoani Lindi, vinakwenda kupatiwa huduma ya umeme,baada ya Kuzinduliwa kwa mradi wa nishati vijijini (REA) awamu ya tatu mzunguko wa pili Mkoani humo.

Uzinduzi huo umefanywa na Naibu Waziri wa Nishati  nishati mhandisi STEPHEN BYABATO katika kijiji cha Narungombe Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi.

Akizungumza katika Uzinduzi huo Naibu Waziri BYABATO amesema lengo la serikali ni kutekeleza mradi huo kwa miezi 18 na hadi kufikia Disemba 2022 vijiji vyote viwe vimepatiwa umeme na kwamba katika awamu hii hakuna kijiji kitakachokuwa kimeachwa.

Aidha,amemuagiza meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi mhandisi KAINDA MUSERU kuhakikisha anahamishia ofisi ya malipo vijijini ili kuwarahisishia na kuwa punguza wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda katika ofisi za makao Makuu ya Mkoa ama Wilaya kufanya huduma za malipo.

Naibu Waziri wa Nishati BYABATO ambaye pia ni mbunge wa Bukoba mjini amewataka wananchi kutunza miundombinu ya umeme ili idumu kwa kuacha tabia ya kuchoma moto nguzo za umeme huku akiwataka watumishi wa Tanesco kuwachukulia hatua wale watakaobainika kuihujumu miundombinu hiyo ya umeme.

Awali akimuwakilisha Mkurugenzi mkuu wa wakala wa nishati vijijini (REA) mratibu wa mradi wa Rea kanda ya kusini mhandisi DANIEL MWANDUPE amesema kwa awamu iliyopita Jumla ya vijiji 332 vilipatiwa umeme na kubakia 192 kati ya 524 ambayo vitapatiwa umeme kwa awamu hii ya tatu mzunguko wa pili kupitia wakandarasi wawili ambapo mmoja (Nakuroi) akihudumia Wilaya ya Kilwa, Lindi vijijini na Ruangwa na mwingine ambaye White City atahudumia Nachingwea na Liwale 

 

Share with Others