Hatua ya Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kutoa amri kuwa Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari inayosimamia shughuli za vyombo vya habari nchini, inapaswa kufanyiwa marekebisho kwa sababu inakiuka haki za binadamu, Katiba ya Nchi na Mkataba wa Afrika Mashariki, ni ushindi muhimu na mkubwa kwa Watanzania na watu wote wapigania haki ndani na nje ya mipaka yetu, ikiweka msingi imara kwa wananchi kupinga udikteta wa matumizi ya sheria kandamizi na kusimamia utawala bora unaoheshimu sheria hususan kwa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki.

1. EACJ IMEAMUAJE

(a) Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari na hukumu yenyewe, Mahakama ya EACJ imetamka kwamba kifungu cha 7(3) cha Sheria ya Vyombo vya Habari kinachoweka masharti ya aina ya habari ambazo zinakatazwa kuchapishwa na wandishi habari na vyombo vya habari, kinakiuka misingi ya Utawala Bora, Demokrasia, Utawala wa Sheria na kuheshimu Haki za Binadamu iliyopo kwenye ibara za 6(d), 7(2) na 8(1)(c) za Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

(b) EACJ imetamka wazi kwamba masharti ya kifungu cha 7(3)(a), (b), (c), (f), (g), (h), (i) na (j) vya Sheria hiyo vinakiuka uhuru wa habari na haki ya kutafuta, kusambaza na kupokea habari.

(c) EACJ imetamka kwamba vifungu vya 19, 20 na 21 vya Sheria vinavyohusu masharti ya uandikishaji wa wandishi, makosa na adhabu za ukiukaji wa masharti hayo, vinakiuka uhuru wa habari na haki ya kutafuta, kusambaza na kupokea habari na ni kinyume na matakwa ya ibara za 6(d), 7(2) na 8(1)(c) ya Mkataba.

(d) EACJ imesema kwamba vifungu vya 35, 36, 37, 38, 39 na 40 vya Sheria hiyo vinavyotengeneza kosa la jinai la kukashifu au kashfa ni kinyume na matakwa ya ibara za 6(d) na 7(2) vya Mkataba.

(e) EACJ imetamka kwamba vifungu vya 50 na 54 vya Sheria hiyo vinavyotengeneza makosa ya jinai ya kuchapisha taarifa za uongo au zisizokuwa na ukweli, kuwa viko kinyume na uhuru wa habari na haki ya kutafuta, kusambaza na kupokea habari, na hivyo kukiuka matakwa ya ibara za 6(d), 7(2) na 8(1)(c) za Mkataba.

(f) EACJ imeendelea kusema kuwa vifungu vya 52 na 53 vya Sheria hiyo vinavyotengeneza makosa ya uchochezi vinakiuka haki ya uhuru wa habari na uhuru wa mawazo na fikra, na hivyo ni kinyume na matakwa ya ibara za 6(d), 7(2) na 8(1)(c) vya Mkataba.

(g) EACJ imetamka kwamba vifungu vya 58 na 59 vya Sheria vinavyompa Waziri wa Habari mamlaka makubwa ya kuzuia uingizaji, usambazaji, uuzaji na uchapishaji wa machapisho na habari mbali mbali vinaleta udhibiti wa vyombo vya habari na kukiuka uhuru wa habari na haki ya kutafuta, kusambaza na kupokea habari, na ni kinyume na masharti ya ibara za 6(d) na 7(2) za Mkataba.

(h) Katika hukumu hiyo EACJ imeielekeza Serikali ya Tanzania kuchukua hatua stahiki za kufuta au kurekebisha vifungu vyote vya Sheria ya Vyombo vya Habari vilivyotolewa uamuzi kwa lengo la kuifanya Sheria kwenda sambamba na matakwa ya ibara za 6(d), 7(2) na 8(1)(c) za Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

2. UZITO WA MAAMUZI YA EACJ NA MAHAKAMA KWA NDANI YA NCHI

(a) Maamuzi ya EACJ yana nguvu kuliko maamuzi ya Mahakama za ndani ya Nchi Wanachama wa EAC.

(i) EACJ imetamka kwamba kwa mujibu wa ibara ya 32(2) ya Mkataba, maamuzi yake kuhusu tafsiri na matumizi ya Mkataba huo "yatakuwa na nguvu juu ya maamuzi ya Mahakama za ndani za Nchi Wanachama kwenye masuala yanayofanana na hayo."

(ii) Hivyo ni wazi kuwa kwa kuamua kwamba vifungu mbali mbali vya Sheria hiyo vinakiuka masharti hayo, maana yake Mahakama za ndani ya Tanzania, kuanzia Mahakama ya Rufaa mpaka Mahakama za Mwanzo, zinatakiwa kufuata msimamo huo wa EACJ katika kuamua kesi za aina hiyo zilizoko mbele yao.

(iii) Hii ina maana kuwa kesi nyingi za uchochezi, kashfa au kutoa taarifa za uongo zilizofunguliwa dhidi ya viongozi wetu wa Chama, wanachama, wafuasi, mashabiki na wapenzi wapenda mabadiliko nchini na wananchi wengine kwa ujumla, chini ya Sheria hiyo, sasa zinatakiwa kuamuliwa kulingana uamuzi huu wa EACJ, na zitafutiliwa mbali.

(b) EACJ imetamka kwamba mtu yeyote anayetaka kufungua mashauri katika Mahakama hiyo hahitaji kupitia, au kumaliza, kwanza taratibu za kimahakama za Nchi Wanachama.

Jambo hili lina uzito wa kipekee kwa sababu mahakama hiyo imeelekeza kuwa mtu yeyote ana haki ya kufungua mashauri moja kwa moja katika EACJ bila kuwekewa vizingiti vya kwenda kwanza kwenye Mahakama za ndani ya nchi yake.

(c) Uamuzi huu wa EACJ unatoa fursa nyingine muhimu katika mapambano ya kudai haki za binadamu, utawala wa sheria, demokrasia na utawala bora ndani ya nchi yetu na katika nchi zingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambako haki za watu zinaminywa na kuporwa na watawala wasioheshimu sheria au wanaotumia sheria kandamizi kujilinda dhidi ya maslahi na matakwa ya wananchi ambao ndiyo wenye nchi.

Sasa wananchi watakuwa na uhuru wa kuamua kwenda kudai haki zao EACJ badala ya Mahakama zetu za ndani.

Hatua hii ni muhimu hasa katika mazingira halisi ya Tanzania ya sasa chini ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano ya CCM ambapo kumekuwa na dalili, vitendo na kauli za  kuingilia uhuru wa Mahakama.

Uamuzi huo wa EACJ umekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania pia, kutoa maamuzi katika shauri la rufaa na. 370/2018 lililohusu Hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomhukumu Robert Wangwe kwenda jela mwaka mmoja na nusu au kulipa faini ya Tsh. 5 milioni kwa kuvunja Sheria ya Makosa ya Mtandao. Mahakama Kuu katika hukumu yake iliweka vigezo na rejea muhimu zitakazotumika kuamua kesi zinazohusu sheria hiyo, ambapo ilionesha kuwa hukumu iliyotolewa awali na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi na. 177/2016, haikuvizingatia wakati ikimtia hatiani Wangwe hivyo ilikuwa na mapungufu.

Hukumu hizi mbili zinapaswa kuwa tahadhari kwa Serikali ya Tanzania ambayo kwa muda sasa, na hasa waziwazi tangu awamu ya tano iingie madarakani, imekuwa ikifanya au kunyamazia vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, kuvunja Katiba ya Nchi na mikataba mbalimbali ambayo nchi imetia saini na kuridhia. Vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika kwa njia mbalimbali ikiwemo utungaji na matumizi ya sheria kandamizi, utoaji wa amri au kauli zilizo kinyume na sheria na vitendo vingine vya ukiukwaji wa taratibu za nchi.

Kama tulivyowahi kusema huko nyuma, nchi yetu si kisiwa. Kila kinachofanywa na Serikali hii kinaangaliwa kwa macho mengi, Watanzania wanaona na dunia inaona, namna haki na utawala bora unavyominywa kupitia sheria zisizotenda haki kama; Sheria ya Vyama  vya Siasa, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari.

Mbali ya kutoa pongezi kwa Mahakama ya Afrika Mashariki, katika shauri hilo na. 2/2017, Mahakama Kuu ya Tanzania (masjala ya Dar es Salaam),  kwa kutoa uamuzi unaoweka rejea ya kisheria kwa ajili ya haki kuonekana ikitendeka pia kwa asasi hizo tatu zilizofungua kesi EACJ (Baraza la Habari Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na  Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu) na mwanaharakati Robert Wangwe aliyekata rufaa Mahakama Kuu baada ya kuhukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi, Chadema inaendelea kutoa wito wa Watanzania wote, kupitia nafasi mbalimbali kusimama kidete bila unyonge kupigania haki, kupinga utungwaji na matumizi ya sheria kandamizi na kulinda utawala bora unaozingatia sheria, kwa ajili ya ustawi wa demokrasia na maendeleo ya watu katika taifa letu.

Imetolewa leo Ijumaa, Machi 29, 2019 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
Chadema
 

Share with Others