Katibu mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula amefumua mfumo wa uongozi katika vyuo vya Afya nchini na kuunganisha vyuo vyote vilivyokaribu na hivyo kufanya vyuo kupungua idadi kutoka vyuo 37 hadi kufikia vyuo 9, hali itayosaidia matumizi mazuri ya rasilimali chache zilizopo katika kuzalisha rasilimali watu.

Hayo yamejiri katika mkutano na wakuu wa vyuo vya Afya 37 vilivyo chini ya wizara hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtumba, Jijini Dodoma.

Dkt. Chaula amesema kuwa, lengo la mkutano huo ni kupanga jinsi ya kuboresha taaluma ndani ya vyuo vya Afya nchini ili kutoa Watumishi bora zaidi jambo litakalosaidia kupunguza vifo visivyokuwa vya lazima kwa kiasi kikubwa.

Dkt. Chaula ameongeza kwa kusema kuwa, mfumo bora wa utawala vyuoni ni muhimili mkubwa na wa msingi katika kuhakikisha mafunzo bora yanatolewa katika vyuo vyetu na wahitimu wanaozalishwa kutoka vyuo hivyo wana umahiri unaokusudiwa katika kutoa huduma za Afya kwa wananchi.

Aidha amesema Wizara imekiri kupokea changamoto za uendeshaji wa mafunzo vyuoni, ikiwemo uchache wa watumishi vyuoni, vifaa vya kufundishia, viwango vya ubora wa wahitimu kushuka, huku akisisitiza mabadiliko ya mfumo wa uongozi yatakuwa chachu ya utatuzi wa changamoto hizo.

Mbali na hayo, Dkt. Chaula amewaasa Viongozi wapya kushughulikia changamoto ya malalamiko kutoka kwa wazazi na wanafunzi wanaosoma vyuoni ikiwemo kukosa kwa baadhi ya haki zao, hali iliyopelekea kwa baadhi ya vyuo kupoteza uaminifu kwa wanafunzi na wazazi.

Nae, Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasiliamali Watu Dkt. Saitore Laizer ametoa wito kwa Wakuu wapya wa vyuo hivyo kufanya kazi kwa ushirikiano baina yao, jambo litalosaidia matumizi mazuri ya rasilimali chache zilizopo katika kuzalisha rasilimali watu.

Share with Others