Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Eng.Joseph Nyamhanga amezitaka halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi kwa kujenga madarasa katika shule za sekondari kwa kutumia fedha za ndani ya Halmashauri zao.

Katibu Mkuu Eng.Nyamhanga ameyasema hayo alipotembelea shule ya sekondari ya Mtanda iliopo Wilaya ya Kilwa ambapo ndani ya miezi mitatu halmashauri hiyo imeweza kujenga jumla ya madarasa 17 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia tatu(300mil) ikiwa ni katika kukabiliana na upungufu wa madarasa uliojitokeza baada ya wanafunzi wengi waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2018 kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari mwaka 2019.

Nichukue nafasi hii kwanza kukupongeza mkurugenzi na timu yako kwa juhudi za haraka ulizochukua katika kukabiliana na tatizo hili, lakini niwaagize wakurugenzi wote nchini kutumia vianzo vyao vya ndani badala ya kusubiri kila kitu kutoka serikali kuu alisema Eng.Nyamhanga.

Katibu mkuu huyo aliongeza kuwa zipo halmashauri zenye uwezo mkubwa wa mapato ya ndani  lakini bado wamekuwa wakisubiri kila kitu waletewe badala kuwa wabunifu.

Pamoja na pongezi hizo pia katibu mkuu aliahidi kumleta mwalimu wa Fizikia katika shule hiyo ambapo kwa sasa pamoja na shule kuwa na walimu wanne wa masomo ya Sayansi lakini hakuna mwalimu hata mmoja wa somo hilo.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg Renatus Mchau amemhakikishia katibu Mkuu kuwa yeye pamoja na timu yake ataendelea kusimamia mapato ya ndani kwa ufasaha ili kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hasa katika sekta za Elimu na Afya.

 

Share with Others