Wadau wa elimu ya awali nchini wamesema mrudindikano wa wanafunzi wa darasa la awali  umekuwa mkubwa,  hali inayowafanya walimu kushindwa kumfikia mwanafunzi mmoja mmoja katika ufundishaji.
 

Wameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa mkutano uliowaandaliwa na serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Tekonolojia pamoja na Tamisemi ukiwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu ya awali wakiwemo asasi za kiraia, vyuo vikuu na waalimu.

Mmoja wa wachangiaji katika mkutano huo, Mwalimu wa darasa katika shule ya msingi Madizini wilayani Mvomero Mkoani Morogoro Monica Kibena amesema, madarasa wanayofundisha yana wanafunzi kuanzia wanafunzi 150 hadi 200 ambao alisema ni mwalimu mmoja hawezi kulimudu darasa .

Kibena amesema,mrundikano huo unawafanya walimu kushindwa kufanya upimaji wa mtoto mmoja mmoja ili kujua uelewa, hivyo ili kuikabili changamoto ni vyema Serikali ijenge madarasa ya kutosha na kuwagawangwa wanafunzi hao kwa uwiano unaotakiwa wa wanafunzi 25 kwa mwalimu mmoja.

Mwalimu Kibena ametumia fursa hiyo pia kuishauri Serikali kuwatumia baadhi ya walimu waliopata mafunzo akiwemo yeye kutoka CIC ambayo yamewezesha kulimudu darasa kubwa .

Aidha Mwalimu Kibena amewataka walimu wenzake kuwa wabunifu kwa kutafuta zana za kufundishia kulingana na mazingira ili kuongeza uelewa wa wanafunzi wanapokuwa shuleni.

Awali Mkurugenzi Mkazi wa shirika linaloshughulika na masuala  ya makuzi na malezi ya awali ya watoto wadogo (CIC) Craig Ferla amesema kuwa  wadau wa elimu wanapaswa kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto za elimu ya awali nchini kulingana na ongezeko la watoto hao.

Bw.Ferla amesema kuwa uandikishaji wa watoto kwa mwaka 2016 umeongezeka hadi kufikia 1.5 milioni kutoka watoto milioni moja mwaka 2015.

Akifungua Kikao hicho kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Elimu Avemaria Semakafu, Mkurugenzi Msaidizi Uendeshaji wa Sera wa wizara hiyo Bw.Yesse Kanyuma aliipongeza Asasi ya CIC kwa kuanzisha mradi huo ambao unawajengea watoto umahiri pamoja na kutoa mbinu za ufundishaji wa watoto wa darasa la awali.

Share with Others