Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameanzisha kampeni maalum ya kuwasaka wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi ya nyumba kwa nyumba na wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi ambao hawajalipa hadi mwaka huu.

Kampeni hiyo ambayo aliizindua mwishoni mwa wiki wilayani Karatu mkoani Arusha, alipokuwa akisikiliza na kutatua migogoro ya ardhi ya wakazi wa wilaya hiyo katika kampeni ya Funguka kwa Waziri, amewaagiza watendaji wote wa wilaya na kanda nchini kuanza kuwasaka nyumba kwa nyumba wadaiwa wa kodi ya ardhi.

“Naagiza mikoa yote ya Tanzania Bara kuanza kampeni rasmi ya kuwasaka wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi ya nyumba kwa nyumba na msiwaonee huruma hata kama ni waziri na anadaiwa kodi ya ardhi peleka mahakamani hata kama ni kiongozi yeyote, hata kama Mkuu wa Wilaya mfuate na peleka mahakamani," alisema Waziri Lukuvi.

Aliwataka wamiliki wote wa ardhi kujitathmini na kukagua taarifa zao kama wamelipa kodi ya ardhi na kuanza kulipa haraka kabla kampeni hiyo haijamfikia mdaiwa.

Aliwataka watendaji wake wasiwe na huruma na mtu yeyote anayedaiwa kodi kwa sababu fedha za kodi ndizo zinazosaidia katika ujenzi wa miundombinu na utoaji huduma kwa wananchi na ndizo zinazosaidia uendeshaji wa serikali kwa kiasi kikubwa.

Share with Others