Kanisa Katoliki Dayosisi ya Erie jimbo la Pennsylvania nchini Marekani limemlipa fidia ya billion 4 mwanaume mmoja kwa kosa la kunyanyaswa kingono na Katekista David Poulson wa Kanisa hilo mwaka 2002.

Mtandao wa Daily Mail umeripoti kuwa, Mitchell Garabedian ambaye ni mwanasheria wa Mwanaume huyo amesema kuwa Kanisa hilo lilimlipa siku ya jumanne kama fidia kutokana na kitendo hicho.

Aidha, David Poulson (65) alihukumiwa miaka 14 kwenda jela mwezi Januari mwaka huu kwa kosa la kulawiti mtoto mwaka 2002 na miaka mingine miwili kwa kosa la kumnyanyasa kingono mtoto mwingine wa kike kwa kumuonyesha picha chafu mwaka 2010.

Licha ya Kanisa hilo kumlipa muathirika bado katekista huyo yupo jela na tayari Vatican mwezi huu Machi imetangaza kumvua hadhi yake ya kutumikia Kanisa hilo kutokana na matendo aliyoyafanya.

Pia mwezi Februari Mwaka huu, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis aliongoza mkutano wa kihistoria, Mjini Vatican, uliojadili jinsi ya kukabiliana na manyanyaso ya ngono dhidi ya watoto, tuhuma ambazo zimekuwa zikilitafuna kanisa kwa miongo kadhaa.

Hata hivyo, Kanisa Katoliki ulimwenguni kote lipo katika vita ya kukomesha kashfa hizo zinalolichafua kanisa hilo kwa kipindi kirefu.

Share with Others