Serikali imewahakikishia wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa hadi kufikia tarehe 31 Machi mwaka huu, wakulima wote wa Korosho watakuwa wamelipwa fedha zao kwani uhakiki umekamilika kwa kiasi kikubwa. 

 Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo JAPHET HASUNGA wakati akitoa ufafanuzi kuhusu malipo hayo kwenye mkutano uliowakutanisha wajumbe wa kamati hiyo kwenye ukumbi wa mikutano katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi. 

Mkutano huo umehusisha kamati hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wake DKT Christine Ishengoma, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Naibu Katibu Mkuu wizara ya  kilimo, wataalamu serikalini sambamba na wakulima. 
Amesema pamoja na kwamba malipo ni mchakato unaohitaji kupitia katika hatua nyingi za kimchakato ikiwemo uhakiki lakini kila jambo lenye mwanzo ni lazima kuwa na ukomo. 
Aidha Waziri HASUNGA amesema mpaka sasa Tani 222,684 zimekwisha kusanywa huku hadi kufikia tarehe 14 Machi 2019 tayari jumla ya Shilingi Bilioni 596.9 zimekwishalipwa kwa wakulima kati ya Shilingi Bilioni 723.
Katika hatua nyingine Waziri HASUNGA ameuagiza uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa viuatilifu Vya Tropiki (TPRI) kutuma wataalamu Mkoani Lindi, kuchukua sampuli za viuatilifu kwa wakulima na kuvipima ili kubaini kadhia ya usambazaji wa viuatilifu batili kwa wakulima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge DKT CHRISTINE ISHENGOMA amemuagiza Waziri HASUNGA kuhakikisha kuwa taarifa ya malipo ya wakulima wote wa Korosho inafika bungeni tarehe 2 Aprili mwaka huu.
 

Share with Others