Rais Magufuli amesema rushwa zinazotozwa na maafisa wa serikali na udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara ni baadhi ya vikwazo vikubwa vinavyoandama ukuaji wa biashara na uchumi nchini Tanzania.

Akizungumza katika mkutano maalum aliouitisha leo na wafanyabiashara zaidi ya 1,000 ambapo kila wilaya ilipeleka wafanyabiashara watano Rais Magufuli amesema japo kuna jitihada kubwa zinazofanyika kupambana na rushwa, bado kuna maafisa wa serikali si waaminifu.

Magufuli ameyataja maeneo yanayoongoza kwa rushwa ni bandarini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), barabarani pamoja na mipakani.

Hii leo, amewaasa wafanyabiashara hao wasisite kuwaripoti maafisa wanaowaomba rushwa kwa mamlaka ili wachukuliwe hatua.

Magufuli pia amekiri kuwa bado serikali haijaweka mipango endelevu ya kuwaendeleza wafanyabiashara na sekta binafsi kwa ujumla wake ili wachangie zaidi kwenye kuujenga uchumi wa nchi.

Pamoja na hayo Rais ametaja utitiri wa kodi na taasisi za udhibiti kama ni chamgamoto nyengine ya kimfumo inayoathiri ukuaji wa biashara nchini Tanzania. Lakini amesema jitihada za kutatua changamoto hiyo zinafanyiwa kazi na wameanza kwa kufuta tozo a ada zaidi ya 100 kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Kwa upande wa wafanyabiashara, Magufuli amesema wapo ambao si waaminifu wanakwepa kodi kwa kutoa rushwa na wengine kufanya udalali na kujihusisha na makundi ya uhalifu wa kibiashara ambapo Magenge hayo amesema yapo katika biashara ya sukari, mafuta ya kula na korosho.

Aidha Rais Magufuli ameongeza kwa kusema moja ya sababu ya suala hilo kuwa kubwa ni udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara.

Tatizo jengine la wafanyabiashara lilogusiwa na Magufuli ni kubadli matumizi ama kutoendeleza kabisa viwanda ama ardhi walizobinafsishiwa na serikali bila kufuata utaratibu.

 

 

Share with Others