Malipo ya Korosho kwa wakulima wilayani Masasi Mkoani Mtwara yametajwa kuwa ni chanzo cha ongezeko la uwepo wa kina dada wanaofanya biashara ya ngono wilayani humo ili kujipatia fedha hizo za korosho.

 Hayo yamesemwa wilayani Masasi na Madiwani wa halmashauri ya mji Masasi walipokuwa wakizungumza  kwa nyakati tofauti kwenye kikao cha baraza la Madiwani.

 Wamesema katika wilaya ya Masasi hivi sasa kumekuwa na makundi mbalimbali ya wasichana kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa ya Tanzania ambao wanafanya biashara ya ngono.

Diwani wa kata ya Mkuti, Hamza Machuma amesema kata yake ya Mkuti kuna makundi ya wasichana ambao wamekodi vyumba mitaani na biashara yao kubwa ni biashara ya ngono.

Amesema wasichana hawa mara nyingi wamekuwa wakionekana hasa katika kipindi cha misimu ya mauzo ya zao la korosho kwa vile wanafahamu kipindi hiki wakulima wanapata fedha za zao hilo.

 Naye diwani wa kata ya Mkomaindo, Ally Salvatory alisema halmashauri isisite kuchukua hatua ili kuwanusuru wakulima wasipoteze fedha zao.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa jimbo la Masasi, Rashidi Chuachua amesema kasi ya wasichana kutoka maeneo mbalimbali kuja Masasi kwa ajili ya kufanyashughuli ya biashara ya ngono ni kubwa na lazima idhibitiwe.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Masasi, Gimbana Ntavyo alisema wataalamu wa halmashauri hiyo wamekuwa wakiwatembelea wakulima kwenye maeneo na kuwapa elimu mbalimbali ikiwemo ya ujasiliamali.

Share with Others