Mfalme Akihito wa Japan amefanya maombi mbele ya Mungu wa Jua "Shinto” leo ikiwa ni mwanzo wa hatua za kumalizika kwa utawala wake wa miaka 30. Mfalme huyo mwenye umri wa miaka 85 alivaa vazi la kijadi alipokwenda Hekalu la Kashikodokoro kuielezea miungu kuhusu kustaafu kwake.


Akihito ndiye wa kwanza wa Japan kuachia madaraka katika muda wa karne mbili. Alisema ilikuwa ni heshima kubwa kwake kutekeleza majukumu yake huku watu wa Japan wakiwa na imani kamili kutokana na uongozi wake.
Hata hivyo Mfalme Akihito atamwachia mamlaka mwanawe Naruhito.


Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini, Kim In Chul, alisema Rais Moon Jae-In amemshukuru Mfalme Akihito kwa kuweka msisitizo juu ya amani na mchango wake juu ya kuendeleza mahusiano mema kati ya Korea ya Kusini na Japan na kwamba alitarajia kuwa mfalme huyo angeliendelea kuunga mkono maendeleo na mahusiano ya nchi hizo mbili hata baada ya kustaafu kwake. 


Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje amesema serikali ya Korea Kusini pia ilimpongeza mfalme mpya, Naruhito, na kuongeza kwamba Korea Kusini inatarajia mahusiano mazuri kati ya nchi mbili hizo yangeliendelea.
Katika sherehe zilizotarajiwa kufanyika kwenye kasri baadaye Jumanne, Mfalme Akihito alitazamiwa kutangaza rasmi kustaafu kwake mbele ya viongozi wa serikali na wana familia ya kifalme.


Hata hivyo, mfalme huyo ataendelea kuwa mtawala hadi saa sita usiku kwa saa za Japan, ambapo mwanawe, Mwana Mfalme Naruhito, atarithi kiti cha enzi siku ya Jumatano (Mei Mosi) na kuwa mfalme mpya.
 

Share with Others