Watanzania wametahadharishwa kuhusu matatizo ya macho na wametakiwa kujiepusha na mambo yanayosababisha ubovu wa viungo hivyo muhimu.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Alibainisha hayo mwishoni mwa wiki katika kambi ya macho ya siku nne iliyoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake ya mkoani Tanga (Tawode) kwa kushirikiana na taasisi ya Kiislamu ya Bilal Muslim Mission ya Tanzania, chini ya udhamini wa taasisi ya Better Charity ya Uingereza.

Ummy ametaja mambo yanayosababisha ubovu wa macho kuwa ni uvaaji wa miwani ya urembo, matumizi ya dawa za macho bila ushauri wa daktari na ulaji wa vyakula ambavyo havina vitamin A.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, katika kila Watanzania 100, wanne kati yao wanasumbuliwa na ubovu wa macho, mmoja anakabiliwa na upofu na watatu kati yao wanasumbuliwa na uoni hafifu na wa kati.

"Ukiona una tatizo la macho nenda kwenye vituo vya afya ukafanyiwe uchunguzi ili upate matibabu haraka, watanzania hakikisheni mnachunguza afya ya macho na afya ya kinywa mara moja kila mwaka," alisema.

Aliongeza "Katika watu 100 wanaokwenda kutibiwa magonjwa ya macho 80 kati yao wanapona, hivyo inapotokea fursa kama hii ichangamkieni."

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Clemence Marcell aliishukuru taasisi hiyo kwa kufanya huduma ya matibabu kwa wakazi wa mkoa wa Tanga bure.

Share with Others