Jackline Samwel (9), amefariki dunia leo Alhamisi Desemba 12, 2019 baada ya kugongwa na gari lililokuwa katika msafara wa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro mkoani Morogoro.


Akizungumza na waandishi leo kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Mugabo Wekwe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, “ni kweli ajali imetokea leo saa 4 asubuhi eneo la Kwa Makunganya.”


Amesema Jackline ni  mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya Msingi Mbwanga mkoani Dodoma, kwamba amegongwa na gari la msafara huo wakati akivuka barabara eneo la Kwa Makunganya manispaa ya Morogoro.


Mashuhuda wa tukio hilo wamesema mwanafunzi huyo aligongwa na gari wakati akivuka barabara baada ya kutoka kununua maji akiwa na mama yake mdogo na ndugu zake wengine watatu.


Wanaeleza kuwa baada ya wenzake kuvuka kurejea katika basi la kampuni ya ABC walilokuwa wakisafiria kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, yeye alikuwa wa mwisho kuvuka  ndipo alipogongwa na gari hilo na kufariki dunia.


Kaimu kamanda huyo amesema mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa Hospitali ya rufaa Mkoa wa Morogoro.
 

Share with Others