Mkuu wa wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai amesema atafuatilia kwa karibu mchakato wa uuzaji na ununuzi wa mazao ya kilimo ya wakulima katika vyama vya msingi vya ushirika vilivyopo wilayani humo.

Akizungumza katika mamlaka ya mji mdogo wa Kilwa Masoko baada ya kukamilika zoezi la kuwalipa wakulima wa ufuta katika vijiji vya Nanjirinji na Zinga ambao walikuwa hawajalipwa kutokana na fedha zao kuibiwa na viongozi na watendaji wa AMCOS, alisema kuanzia sasa atakuwa anafutilia kwakaribu zaidi mchakato wa ununuzi na uuzaji wa mazao ya kilimo kwenye AMCOS zote zilizopo wilayani Kilwa.

Ngubiagai amesema atafanya ziara za kushitukiza za mara kwa mara kwenye ofisi za AMCOS wilayani humo na kusema amejifunza mengi kupitia zoezi linaloongozwa na kaimu mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo dhidi ya viongozi wa AMCOS walioiba fedha za wakulima wa ufuta. Ambao baadhi yao wameanza kurejesha nakusababisha wakulima kuanza kulipwa.

Pamoja na hayo Mkuu huyo wa wilaya ya Kilwa amewataka watumishi wa umma wenye wajibu wa kusimamia, kukusanya mapato na kudhibiti mianya ya uvujaji mapato watimize wajibu wao kikamilifu. Pia amewaonya watumishi wa umma watakao bainika kushirikiana na viongozi na watendaji waovu wa AMCOS na watakaoshindwa kusimamia kikamilifu wajibu wao watalazimika kubeba machungu ya matendo na uzembe wao. Huku akisisitiza kwamba hilo sio ombi bali agizo na hana muda wa wakuwambeleza watumishi watimize wajibu wao.

Share with Others