Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewasilisha muswada katika Baraza la Wawakilishi unaolenga kufuta na kuandika upya sheria ya vileo, na kuweka masharti ya kudhibiti na kusimamia uagizaji, uhifadhi, uuzaji, usambazaji na unywaji pombe

Kwa mujibu wa muswada huo, hakuna mtu anayeruhusiwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza pombe Zanzibar na atakayeivunja atahukumiwa kifungo cha miaka isiyopungua mitano au kulipa faini isiyopungua TZS 5M, huku mitambo yake ya kuzalisha pombe ikitaifishwa.

Akizungumza kwa simu, Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii (Zati), Seif Miski amesema hivi karibuni kumekuwa na baa nyingi zilizofunguliwa katika maeneo ya vijijini zinazosababisha usumbufu na kusema kuwa sheria hiyo itahusika kwa watu wanaoingiza, wanaohifadhi, wanaouza, wanaosambaza na kutumia pombe visiwani Zanzibar.

Aidha muswada huo utazuia kutoa leseni ya kuuza au ruhusa ya maghala au uingizwaji wa vileo au kutolewa leseni Zanzibar kwa wazalishaji wa pombe au kwa mtu yeyote atakayekuwa na mkataba wa kuingiza au kuuza pombe hata hivyo sheria hiyo ikipitishwa itawadhibiti watu kunywa au kukaribia maeneo ya aina yoyote ya vileo visiwani Zanzibar.

Pia, unakataza mtu yeyote, idara ya Serikali au taasisi yoyote kuuza au kutunza vileo vinavyochochea ulevi bila kuwa na leseni au kuweka ghala la vileo.

Kwa hali hiyo, mtu atakuwa na hatia ya kukutwa na kileo, isipokuwa mtu aliye na leseni chini ya sheria hiyo au mtu aliyenunua na kumiliki kileo hicho iwe ni kwa matumizi binafsi au kwa biashara.

Muswada huo utakaoendelea kujadiliwa kesho, unaanzisha Bodi ya kuzuia na kudhibiti vileo itakayokuwa na mamlaka ya kutoa vibali kwa mujibu wa sheria, kwa hoteli, baa, maduka, maghala na vibali vya kusambaza vileo katika matukio muhimu.

Sheria hiyo inazuia mtu kuonekana kutoka kwenye baa akiwa ameshika kileo na imeweka masharti mbalimbali ya kumiliki leseni za vileo visiwani humo, yote ikiwa ni katika kupambana na vitendo vya vurugu vinavyosababishwa na walevi wa pombe.

Share with Others