Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jeshi la Magereza nchini ukamilishe mkakati wa ujenzi wa magereza za wilaya kwa wilaya zisizokuwa na magereza.

Ametoa agizo hilo wakati akifungua Gereza la wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. Uzinduzi huo umefanyika kwenye viwanja vya gereza hilo.

Waziri Mkuu amesema uwepo wa magereza katika wilaya zote nchini utasaidia kumaliza tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza ya jirani.

“Kutokuwepo kwa magereza ya wilaya kunasababisha msongamano wa wafungwa na mahabusu katika magereza ya jirani, pamoja na kuchelewesha upatikanaji wa haki.”

Waziri Mkuu amesema kwamba ufunguzi wa gereza la Ruangwa utatatua tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza la wilaya ya Nachingwea.

Awali wakazi wa wilaya hiyo waliokabiliwa na tuhuma mbalimbali au waliohukumiwa vifungo walikuwa wakipelekwa katika Gereza la wilaya ya Nachingwea.

Amesema kitendo cha kupelekwa Nachingwea kilikuwa kikiwanyima wafungwa na mahabusu fursa ya kuonana na ndugu au mawakili wao kutokana na umbali uliokuwepo.

“Mbali na ndugu na jamaa kushindwa kwenda kuwaona ndugu zao pia Jeshi la Polisi lilikuwa likilaumiwa kuwa linawachelewesha mahubusu kuja kusikiliza mashauri yao.”

Waziri Mkuu amesema uwepo wa gereza hilo katika wilaya ya Ruangwa umeipunguzia Serikali gharama za kuwasafirisha mahabusu na wafungwa kwenda Nachingwea.

Awali, Waziri waMambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema Gereza la Wilaya ya Ruangwa ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wilaya hiyo.

Share with Others