Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2019 yameanza hii leo jijini Dodoma, yakilenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari.


Msisitizo mkubwa umetolewa kwa wadau wa habari kujadili viashiria vya kushuka kwa uhuru vya habari nchini Tanzania na namna ya kuviepuka hususani baadhi ya waandishi wa habari kupotea, kukamatwa na kushikiliwa kwa muda na mamlaka nchini.

Aidha wanahabari pamoja na wahariri wamepewa changamoto ya kuhoji sababu za Tanzania kushuka kwa nafasi 25 kutoka nafasi ya 93 mwaka jana hadi nafasi ya 118 mwaka huu kwenye orodha ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.


“Tunapaswa kuhoji kwa nini tumeshuka kwenye nafasi ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, mwaka jana tulishuka kwa nafasi 10 kutoka nafasi ya 73 hadi nafasi ya 93 na mwaka huu tumeshuka kutoka nafasi ya 93 hadi nafasi ya 118”, wamehoji washiriki kwenye maadhimisho hayo.

Mkurugenzi wa MISA Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa amesisitiza waandishi wa Habari Tanzania kuongeza kiwango chao cha elimu ili kuendana na matakwa ya sheria hatua itakayosaidia kufanya shughuli zao kwa mujibu wa taaluma bila vikwazo kutoka kwa mamlaka za kisheria.


Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya elimu (UNESCO) nchini Tanzania, Nancy Kaizirege amesema waandishi wa habari wanapaswa kushikamana pamoja ili kulinda usalama wao.


“Waandishi 99 waliuawa mwaka jana wakiwa kazini na tangu mwaka 1994 hadi 2018 jumla ya waandishi 1,377 wameuawa kutokana na majukumu hayo”, amebainisha Kaizirege akieleza jinsi usalama wa waandishi wa habari ulivyo mashakani.


Taasisi mbalimbali zimeshiriki kwenye maandalizi ya maadhimisho hayo ikiwemo MISA Tanzania, Internews, IMS, UTPC, TMF, TEF, UK Aid, TAMWA, MCT, UN Tanzania, FES, Unesco na Serikali ya Tanzania, kauli mbiu ya kimataifa ikiwa ni “Vyombo vya Habari kwa Demokrasia, Tasnia ya Habari na Uchaguzi nyakati za upotoshwaji wa taarifa”  huku Nchini Tanzania tukisema "Jukumu la Umoja wa Klabu za waandiahi wa Habari Tanzania na Klabu za waandishi wa habari kuchangia uchaguzi huru na haki" ambapo kilele cha maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka Mei 03.

Share with Others