Serikali kwa kushirikiana na taasisi za sekta binafsi imeendelea kutoa elimu ya kilimo bora inayojumuisha matumizi sahihi ya mbolea za asili, viuatilifu vya asili, mbegu bora na hifadhi ya mazingira ili kuzalisha mazao kwa tija na kuwa na kilimo endelevu.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Chambani Mhe Yussuf Salim Hussein aliyetaka kufahamu Serikali imeweka mikakati gani ya kutoa elimu ya mbolea ya asili kwa wakulima na hatua Serikali inayoichukua ili kuona kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kuzalisha mazao yasiyotumia mbolea za viwandani.

Alisema kuwa katika kutekeleza mpango wa muda mrefu wa matumizi sahihi ya virutubisho vya udongo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) inafanya utafiti wa afya ya udongo katika Kanda zote saba za kiikolojia za kilimo nchini.

Utafiti huo unalenga kubaini aina za virutubisho na tabia za udongo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kiasi, aina na matumizi sahihi ya mbolea za viwandani na asili.

Utafiti huo umeanza kwa kuchukua sampuli za udongo katika Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini na sehemu ya Kanda ya Mashariki (Mkoa wa Morogoro) na utaendelea katika maeneo mengine nchini na kukamilika Juni 2020.

Alisema, kwa kutambua ongezeko la mahitaji ya mazao na bidhaa za kilimo zinazozalishwa kwa kutumia mbolea za asili na viuatilifu vya asili, Serikali imeboresha mtaala wa mafunzo katika vyuo vya kilimo ambapo mada za kilimo hai na hifadhi ya mazingira zimejumuishwa ili kuwawezesha maafisa ugani na wakulima kupata elimu hiyo.

Aidha, alisema kutokana na umuhimu wa wanawake katika kilimo Serikali imeielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) katika mikopo inayotoa asilimia 20 ya mikopo itolewe kwa vikundi vya wanawake. Hadi Januari 2019, asilimia 33 ya mikopo imetolewa katika vikundi vya wanawake kupitia Benki ya TADB. 

Mhe Mgumba aliongeza kuwa, Serikali imeuelekeza Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (Agricultural Input Trust Fund – AGITF) kutoa kipaumbele kwa vikundi vya wanawake vinavyoomba mikopo ya kuendeleza kilimo. Vile vile, Serikali imeendelea kutoa hati miliki za ardhi za kimila na hati miliki za ardhi kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi na kuzitumia kama dhamana kukopa katika taasisi mbalimbali za kifedha ili waweze kupata mitaji ya kununua pembejeo na zana bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji, tija na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa mazao ya kilimo.

Share with Others