Zaidi ya wananchi 4500 wa vijiji sita wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi hawana mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai amevitaja vijiji hivyo kuwa ni Kiranjeranje, Nanjilinji A, Ruatwe, Njinjo, Nakiu na Nanjilinji B.

Amesema mbali na nyumba kubomoka, mashamba na mifugo ya wananchi hao pia imesombwa na maji.

Ngubiagai amesema timu ya uokoaji imekwenda eneo lililokumbwa na mafuriko kwa boti kunusuru maisha ya wananchi na kwamba wananchi hao watapelekwa katika maeneo yaliyotengwa huku akiwataka watu wa kada mbalimbali kutoa msaada kwa wananchi hao.

“Tunaendelea kuwaokoa na kuwapeleka maeneo ambayo tumeyatenga. Tunahitaji msaada wa chakula, dawa, nguo na vitu vingine muhimu,” amesema Ngubiagai.

Mapema siku ya jana akiwa mpakani mwa wilaya ya Liwale na Nachingwea , Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi alisema tayari watu wanne wamefariki kwa wilaya ya Kilwa watu wawili na wilaya ya Ruangwa watu wawili kutokana na mvua hizo huku akiwaomba wanachi mkoani humo kuacha kutembea wakati wa usiku na kuchukua tahadhari kwani hali ni mbaya mno 

 

 

Share with Others