Kundi linalojiita dola la Kiislamu IS, kupitia chombo chake cha habari cha AMAQ, limekiri kuwaua wanajeshi 11 nchini Nigeria katika shambulio Kaskazini Mashariki mwa mji wa Gajiganna.

 

Kundi hilo limesema liliwashambulia wanajeshi hao siku ya Ijumaa na kuonesha picha za miili ya wanajeshi waliokufa katika shambulio hilo. Katika tukio hilo wanamgambo wa kundi hilo walizingira mji wakiwa na pikipiki majira ya saa kumi na mbili unusu jioni na kuanza kuwafyatulia risasi raia na wanajeshi.

 

Kundi la dola la Kiislamu Magharibi mwa Afrika ISWAP limekuwa likifanya mashambulizi mfululizo katika miezi ya hivi karibuni nchini Nigeria. Kundi hilo lilijitenga mwaka 2016 na kundi la Boko Haramu, ambalo liliendesha uasi kwa muongo mzima kaskazini-magharibi mwa Nigeria, ambapo watu karibu 30,000 wameuawa na wengine milioni 2 kuyapa kisogo makaazi yao.

Share with Others