Mkuu wa mkoa wa Lindi,Godfrey Zambi amemuagiza kamanda wa Polisi wa mkoa (RPC), wa mkoa huo ahakikishe waliokuwa viongozi wa Chama Cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) cha Mbwemkuru, kilichopo katika wilaya ya Liwale wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Zambi alitoa agizo hilo jana wakati wa kikao cha tathimini ya ununuzi wa korosho kwa msimu wa 2018/2019 na maandalizi ya ununuzi wa ufuta msimu wa 2019/2020. Kikao ambacho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi.

Zambi alisema watu hao wanatakiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria(washitakiwe) ili wakajibu shitaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. Kutokana na kushindwa kuipa tani 35 na kilo 395 za ufuta kampuni ya Hyseas International Investment(T) Ltd ambayo ilinunua zao hilo katika chama cha Mbwemkuru, msimu wa 2018/2019 kwa thamani ya shilingi 101,187,226.

Alisema wakamatwe na washitakiwe  kama wahalifu wengine, hata kama bodi ya chama hicho ilivunjwa na watu hao kuwa nje ya uongozi. Kwani bado wanakabiliwa na tuhuma hizo ambazo ni mahakama pekee inaweza kutoa haki.

"Suala la kwamba yalifanyika makubaliano kwamba watalipa halipo.  Nataka hadi tarehe 5,mwezi Mei,mwaka huu(2019) niletewe taarifa ya utekelezaji wa agizo hili," alisisitiza Zambi.

Alisema kutowachukulia hatua za kisheria viongozi wenye tabia hiyo kutawatisha wanunuzi na kusababisha malalamiko ya mara kwa mara ya wanunuzi kutapeliwa. Lakini pia ni chanzo cha kuvisababishia hasara vyama vya ushirika.

 

Share with Others